Ulinganishi wa Mzizi wa Vitenzi katika Lugha ya Kiswahili na Kiarabu.
Abstract
Ikisiri
Makala hii imelenga kuchambua ulinganishaji wa mzizi wa vitenzi katika lugha ya Kiswahili na Kiarabu. Vitenzi vinavyochambuliwa katika makala hii ni vitenzi vikuu vya lugha husika. Katika uchambuzi huo, makala hii, kwanza imeeleza kwa muhutasari uhusiano uliopo baina ya lugha ya Kiswahili na Kiarabu kwa ujumla wake kisha kufafanua dhana ya vitenzi inavyojitokeza kwenye lugha ya Kiswahili na Kiarabu. Sambamba na hilo makala imeeleza dhana ya mzizi na namna unavyojitokeza pamoja na aina zake kwa mifano. Nadharia ya Umbo Upeo iliyoasisiwa na Prince na Smolensky mwaka (1993) ndio iliyoongoza uchanganuzi wa data katika kuangalia mzizi wa vitenzi katika lugha ya Kiswahili na Kiarabu. Makala imebaini kwamba lugha ya Kiarabu na Kiswahili zinatofautiana sana katika utokeanji wa mzizi wa vitenzi. Hii ina maana kwamba mzizi wa vitenzi vya Kiswahili hutengana na mofimu tamati kama maumbo mawili yanayojitegemea wakati mzizi wa vitenzi vya Kiarabu huungana na mofimu tamati kama umbo moja. Hivyo makala imehitimisha kwa kusema kwamba kuna tofauti kubwa ya namna mzizi wa vitenzi vya lugha ya Kiswahili vinavyojitokeza na uundaji wake ukilinganisha na mzizi wa vitenzi vya lugha ya Kiarabu.